Wafuatao ni watu wa mkoani waliotoka utumwani ambao Nebukadneza mfalme wa Babuloni aliwapeleka mateka Babuloni, wakarudi mjini Yerusalemu na nchini Yuda. Kila mtu alirudi mjini kwake.
Viongozi wao walikuwa Zerubabeli, Yeshua, Nehemia, Seraya, Reelaya, Mordekai, Bilshani, Mispari, Bigwai, Rehumu na Baana. Ifuatayo ni idadi ya watu wote wa koo za Israeli waliorudi kutoka uhamishoni:
Watu wa miji ifuatayo, pia walirudi: Wa mji wa Tel-mela, wa Tel-harsha, wa Kerubu, wa Adani na wa Imeri, ila hawakuweza kuthibitisha kuwa walikuwa wazawa wa Waisraeli.
Watu wa koo zifuatazo za makuhani pia walirudi: Ukoo wa Habaya, wa Hakosi na wa Barzilai. Huyo Barzilai alikuwa ameoa binti Barzilai wa Gileadi, naye pia akaitwa Barzilai.
Watu hao waliotoka uhamishoni, walipofika kwenye nyumba ya Mwenyezi-Mungu mjini Yerusalemu, baadhi ya viongozi wa koo hizo walitoa matoleo ya hiari ili kusaidia ujenzi wa nyumba ya Mungu katika Yerusalemu.
Walitoa kila mtu kadiri ya uwezo wake kwa ajili ya kazi hii. Jumla ya matoleo hayo ilikuwa kilo 500 za dhahabu, kilo 2,800 za fedha na mavazi 100 kwa ajili ya makuhani.
Basi, makuhani, Walawi na baadhi ya watu wengine wakaanza kuishi mjini Yerusalemu na katika vitongoji vyake. Nao waimbaji, walinzi wa hekalu na watumishi wa hekalu wakaanza kuishi katika miji yao; Waisraeli wote waliishi katika miji yao.