Kisha bwana akamwambia Musa, “Ondoka mahali hapa, wewe pamoja na hao watu uliowapandisha kutoka Misri, mpande mpaka nchi niliyomwahidi Ibrahimu, Isaka na Yakobo kwa kiapo, nikisema, ‘Nitawapa wazao wenu nchi hii.’
Pandeni mwende katika nchi itiririkayo maziwa na asali. Lakini mimi sitakwenda pamoja nanyi, kwa sababu ninyi ni watu wenye shingo ngumu, nisije nikawaangamiza njiani.”
Kwa kuwa bwana alikuwa amemwambia Musa, “Waambie Waisraeli, ‘Ninyi ni watu wenye shingo ngumu. Kama ningefuatana nanyi hata kwa muda mfupi, ningewaangamiza. Sasa vueni mapambo yenu, nami nitaamua nitakalowatendea.’ ”
Basi Musa alikuwa na desturi ya kuchukua hema na kuliweka wakfu nje ya kambi umbali kiasi, akaliita “Hema la Kukutania.” Kila aliyekuwa akiulizia shauri kwa bwana, angelikwenda katika Hema la Kukutania nje ya kambi.
Wakati wowote Musa alipokwenda kwenye Hema, watu wote waliinuka na kusimama kwenye maingilio ya mahema yao, wakimwangalia Musa mpaka aingie kwenye Hema.
Kila mara watu walipoona hiyo nguzo ya wingu ikiwa imesimama kwenye ingilio la hema, wote walisimama wakaabudu, kila mmoja kwenye ingilio la hema lake.
bwana angezungumza na Musa uso kwa uso, kama vile mtu azungumzavyo na rafiki yake. Kisha Musa angerudi kambini, lakini msaidizi wake kijana Yoshua mwana wa Nuni hakuondoka mle Hemani.
Musa akamwambia bwana, “Umekuwa ukiniambia, ‘Ongoza watu hawa,’ lakini hujanifahamisha ni nani utakayemtuma pamoja nami. Umesema, ‘Ninakujua wewe kwa jina lako, nawe umepata kibali mbele zangu.’
Mtu yeyote atajuaje kuwa mimi pamoja na watu wako tumepata kibali mbele zako, usipokwenda pamoja nasi? Ni nini kingine kitakachoweza kututofautisha mimi na watu wako miongoni mwa watu wengine wote walio katika uso wa dunia?”
Ndipo bwana akasema, “Nitapitisha wema wangu wote mbele yako, nami nitalitangaza Jina langu, bwana, mbele ya uso wako. Nitamrehemu yeye nimrehemuye, na pia nitamhurumia yeye nimhurumiaye.”