Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Watu wa Moabu wametenda dhambi tena na tena, kwa hiyo sitaacha kuwaadhibu. Wamemkosea heshima marehemu mfalme wa Edomu kwa kuichoma moto mifupa yake ili kujitengenezea chokaa!
Basi, nitaishushia moto nchi ya Moabu, na kuziteketeza kabisa ngome za mji wa Keriothi. Wanajeshi watakapopaza sauti zao na kupiga tarumbeta, watu wa Moabu watakufa katika makelele hayo ya vita.
Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Watu wa Yuda wametenda dhambi tena na tena, kwa hiyo sitaacha kuwaadhibu. Wamepuuza sheria zangu, wala hawakufuata amri zangu. Wamepotoshwa na miungu ileile waliyoihudumia wazee wao.
Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Waisraeli wametenda dhambi tena na tena, kwa hiyo sitaacha kuwaadhibu. Wamewauza watu waaminifu kwa kuwa hawakuweza kulipa madeni yao; na kuwauza watu fukara wasioweza kulipa deni la kandambili.
Huwanyanyasa na kuwakandamiza wanyonge, na maskini huwabagua wasipate haki zao. Mtu na baba yake hulala na mjakazi yuleyule, hivyo hulitia unajisi jina langu takatifu.
Popote penye madhabahu, watu hulalia nguo walizotwaa kwa maskini kama dhamana ya madeni yao; na katika nyumba ya Mungu wao hunywa divai waliyotwaa kwa wadeni wao.
“Hata hivyo, enyi watu wangu, kwa ajili yenu, niliwaangamiza kabisa Waamori ambao walikuwa wakubwa kama mierezi, wenye nguvu kama miti ya mialoni. Naam, niliwaangamiza, matawi na mizizi.
Niliwateua baadhi ya wana wenu wawe manabii, na baadhi ya vijana wenu wawe wanadhiri. Je, enyi Waisraeli, haya nisemayo si ya kweli? Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.