Habari Njema 2001
|
| 1 |
| Lakini jambo hilo halikumpendeza Yona hata kidogo, akakasirika sana. |
| 2 |
| Kwa hiyo akaomba, “Mwenyezi-Mungu, je, hayo si mambo yaleyale niliyowaza utayafanya nilipokuwa nyumbani? Ndio maana nilifanya haraka kukimbilia Tarshishi. Nilijua kwamba wewe u Mungu wa upendo na huruma. Hukasiriki upesi, daima u mwema na u tayari kubadili nia yako wakati wowote ili usiadhibu. |
| 3 |
| Basi, sasa ee Mwenyezi-Mungu, nakusihi uniondolee uhai wangu, maana, kwangu mimi ni afadhali kufa kuliko kuishi.” |
| 4 |
| Naye Mwenyezi-Mungu akamjibu Yona: “Unadhani wafanya vema kukasirika?” |
| 5 |
| Ndipo Yona akatoka nje ya mji, akajikalia upande wa mashariki wa mji huo. Hapo, akajijengea kibanda, akaketi kivulini mwake huku anangojea apate kuona litakaloupata mji wa Ninewi. |
| 6 |
| Mungu, Mwenyezi-Mungu akaamuru mmea uote na kukua. Akauotesha ili kumpatia Yona kivuli cha kumpunguzia taabu aliyokuwa nayo. Yona akaufurahia sana mmea huo. |
| 7 |
| Lakini siku ya pili, kulipopambazuka, Mungu akaamuru mdudu auharibu mmea huo, ukanyauka. |
| 8 |
| Jua lilipochomoza, Mungu akaleta upepo wa hari kutoka mashariki, jua likamchoma sana Yona kichwani, karibu azirai. Yona akasema, “Afadhali kufa kuliko kuishi!” |
| 9 |
| Lakini Mungu akamwambia Yona, “Je, unadhani wafanya vema kuukasirikia mmea huo?” Yona akajibu, “Ndiyo, nafanya vema kukasirika — kukasirika hata kufa!” |
| 10 |
| Hapo Mungu akamwambia, “Mmea huu uliota na kukua kwa usiku mmoja, na usiku uliofuata ukanyauka. Wewe hukuufanyia kitu chochote, wala hukuuotesha. Mbona unauhurumia? |
| 11 |
| Je, haifai kwangu kuuhurumia mji wa Ninewi, ule mji mkuu wenye watu 120,000, wasioweza kupambanua jema na baya, na pia wanyama wengi?” |
| Hifadhi Vidokezo |
https://beblia.bible:81/BibleAudio/swahili2001/jonah/004.mp3
4
4