kabla ya wakati ulioamriwa haujafika na siku ile inayopeperusha kama makapi, kabla hasira kali ya bwana haijaja juu yenu, kabla siku ya ghadhabu ya bwana haijaja juu yenu.
Mtafuteni bwana, enyi nyote wanyenyekevu wa nchi, ninyi ambao hufanya lile analoamuru. Tafuteni haki, tafuteni unyenyekevu; labda mtahifadhiwa siku ya hasira ya bwana.
Ole wenu ninyi ambao mnaishi kando ya bahari, enyi Wakerethi; neno la bwana liko dhidi yenu, ee Kanaani, nchi ya Wafilisti. “Mimi nitawaangamiza, na hakuna atakayebaki.”
Itakuwa mali ya mabaki ya nyumba ya Yuda, hapo watapata malisho. Wakati wa jioni watajilaza chini katika nyumba za Ashkeloni. bwana Mwenyezi Mungu wao atawatunza, naye atawarudishia wafungwa wao.
Hakika, kama niishivyo,” asema bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, “hakika Moabu itakuwa kama Sodoma, Waamoni kama Gomora: mahali pa magugu na mashimo ya chumvi, nchi ya ukiwa milele. Mabaki ya watu wangu watawateka nyara; mabaki ya taifa langu watarithi nchi yao.”
Makundi ya kondoo na ng’ombe yatajilaza pale, viumbe vya kila aina. Bundi wa jangwani na bundi waliao kwa sauti nyembamba wataishi juu ya nguzo zake. Mwangwi wa kuita kwao utapita madirishani, kifusi kitakuwa milangoni, boriti za mierezi zitaachwa wazi.
Huu ndio mji uliotukuka na kuishi kwa furaha wakijisikia salama. Ulisema moyoni mwako, “Mimi ndimi, na wala hapana mwingine ila mimi.” Jinsi gani umekuwa gofu, mahali pa kulala wanyama pori! Wote wanaopita kando yake wanauzomea na kutikisa mkono kwa dharau.