Lakini sasa uwe imara, ee Zerubabeli,’ asema bwana. ‘Kuwa imara, ee kuhani mkuu Yoshua mwana wa Yehosadaki. Mwe imara, enyi watu wote wa nchi,’ asema bwana, ‘na mfanye kazi. Kwa kuwa mimi nipo pamoja nanyi,’ asema bwana Mwenye Nguvu Zote.
Nitatikisa mataifa yote, nacho kile kinachotamaniwa na mataifa yote kitakuja, nami nitaujaza utukufu katika nyumba hii,’ asema bwana Mwenye Nguvu Zote.
‘Utukufu wa nyumba hii ya sasa utakuwa mkubwa kuliko utukufu wa ile nyumba ya mwanzoni,’ asema bwana Mwenye Nguvu Zote. ‘Na mahali hapa nitawapa amani,’ asema bwana Mwenye Nguvu Zote.”
Kama mtu akibeba nyama iliyowekwa wakfu katika pindo la vazi lake, kisha lile pindo likagusa mkate au mchuzi, divai, mafuta au chakula kingine, je, kitu hicho kitakuwa kimewekwa wakfu?’ ” Makuhani wakajibu, “La hasha.”
Kisha Hagai akasema, “Je, kama mtu aliyetiwa unajisi kwa kugusa maiti akigusa mojawapo ya vitu hivi, kitu hicho kitakuwa kimetiwa unajisi?” Makuhani wakajibu, “Ndiyo, huwa kimenajisiwa.”
Kisha Hagai akasema, “ ‘Basi ndivyo walivyo machoni pangu hawa watu na taifa hili,’ asema bwana. ‘Lolote wafanyalo na chochote watoacho hapo ni najisi.
“ ‘Sasa fikirini kwa uangalifu kuanzia leo na kuendelea: tafakarini jinsi mambo yalivyokuwa kabla halijawekwa jiwe moja juu ya lingine katika Hekalu la bwana.
Wakati mtu alipoendea lundo la nafaka la vipimo ishirini, kulikuwa na vipimo kumi tu. Wakati mtu alipoendea pipa la mvinyo ili kuchota vipimo hamsini, kulikuwa na vipimo ishirini tu.
Je, bado kuna mbegu iliyobakia ghalani? Mpaka sasa, hakuna mzabibu au mtini, mkomamanga wala mzeituni uliozaa tunda. “ ‘Kuanzia leo na kuendelea, nitawabariki.’ ”
Nitapindua viti vya enzi vya falme, na kuziharibu kabisa nguvu za falme za kigeni. Nitapindua magari ya vita pamoja na waendeshaji wake; farasi na wapanda farasi wataanguka, kila mmoja kwa upanga wa ndugu yake.
“ ‘Katika siku ile,’ asema bwana Mwenye Nguvu Zote, ‘nitakuchukua wewe, mtumishi wangu Zerubabeli mwana wa Shealtieli,’ asema bwana. ‘Nitakufanya kama pete yangu ya muhuri, kwa kuwa nimekuchagua,’ asema bwana Mwenye Nguvu Zote.”