Kiswahili Biblia 2005
|
| 1 |
| Akatoka huko, akafika mpaka nchi ya kwao; wanafunzi wake wakamfuata. |
| 2 |
| Na ilipokuwa sabato, alianza kufundisha katika sinagogi; wengi waliposikia wakashangaa, wakisema, Huyu ameyapata wapi haya? Na, Ni hekima gani hii aliyopewa huyu? Na, Ni nini miujiza hii mikubwa inayotendeka kwa mikono yake? |
| 3 |
| Huyu si yule seremala, mwana wa Mariamu, na ndugu yao Yakobo, na Yose, na Yuda, na Simoni? Na maumbu yake hawapo hapa petu? Wakajikwaa kwake. |
| 4 |
| Yesu akawaambia, Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake mwenyewe, na kwa jamaa zake, na nyumbani mwake. |
| 5 |
| Wala hakuweza kufanya mwujiza wo wote huko, isipokuwa aliweka mikono yake juu ya wagonjwa wachache, akawaponya. |
| 6 |
| Akastaajabu kwa sababu ya kutokuamini kwao. Akazunguka-zunguka katika vile vijiji, akifundisha. |
| 7 |
| Akawaita wale Thenashara, akaanza kuwatuma wawili wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu; |
| 8 |
| akawakataza wasichukue kitu cha njiani isipokuwa fimbo tu; wala mkate, wala mkoba, wala pesa za bindoni; |
| 9 |
| lakini wajifungie viatu; akasema, Msivae kanzu mbili. |
| 10 |
| Akawaambia, Mahali po pote mtakapoingia katika nyumba, kaeni humo hata mtakapotoka mahali pale. |
| 11 |
| Na mahali po pote wasipowakaribisha ninyi wala kuwasikia, mtokapo huko, yakung'uteni mavumbi yaliyo chini ya miguu yenu, kuwa ushuhuda kwao. |
| 12 |
| Wakatoka, wakahubiri kwamba watu watubu. |
| 13 |
| Wakatoa pepo wengi, wakapaka mafuta watu wengi waliokuwa wagonjwa, wakawapoza. |
| 14 |
| Naye Mfalme Herode akasikia habari; kwa maana jina lake lilikuwa kutangaa, akasema, Yohana Mbatizaji amefufuka katika wafu, na kwa hiyo nguvu hizi zinatenda kazi ndani yake. |
| 15 |
| Wengine walisema, Ni Eliya. Wengine walisema, Huyu ni nabii, au ni kama mmoja wa manabii. |
| 16 |
| Lakini Herode aliposikia, alisema, Yohana, niliyemkata kichwa, amefufuka. |
| 17 |
| Kwa maana Herode mwenyewe alikuwa ametuma watu, akamkamata Yohana, akamfunga gerezani, kwa ajili ya Herodia, mkewe Filipo ndugu yake, kwa kuwa amemwoa; |
| 18 |
| kwa sababu Yohana alimwambia Herode, Si halali kwako kuwa na mke wa nduguyo. |
| 19 |
| Naye yule Herodia akawa akimvizia, akataka kumwua, asipate. |
| 20 |
| Maana Herode alimwogopa Yohana; akimjua kuwa ni mtu wa haki, mtakatifu, akamlinda; na alipokwisha kumsikiliza alifadhaika sana; naye alikuwa akimsikiliza kwa furaha. |
| 21 |
| Hata ilipotokea siku ya kufaa, na Herode, sikukuu ya kuzaliwa kwake, alipowafanyia karamu wakubwa wake, na majemadari, na watu wenye cheo wa Galilaya; |
| 22 |
| ndipo binti yake yule Herodia alipoingia, akacheza, akampendeza Herode na wale walioketi pamoja naye karamuni. Mfalme akamwambia yule kijana, Niombe lo lote utakalo, nitakupa. |
| 23 |
| Akamwapia, Lo lote utakaloniomba nitakupa, hata nusu ya ufalme wangu. |
| 24 |
| Basi akatoka, akamwuliza mamaye, Niombe nini? Naye akasema, Kichwa cha Yohana Mbatizaji. |
| 25 |
| Mara akaingia kwa haraka mbele ya mfalme, akaomba akisema, Nataka unipe sasa hivi katika kombe kichwa cha Yohana Mbatizaji. |
| 26 |
| Mfalme akafanya huzuni sana, lakini kwa ajili ya viapo vyake, na kwa ajili ya hao walioketi karamuni, hakutaka kumkatalia. |
| 27 |
| Mara mfalme akatuma askari, akaamuru kuleta kichwa chake. Basi akaenda, akamkata kichwa mle gerezani, |
| 28 |
| akakileta kichwa chake katika kombe, akampa yule kijana, naye yule kijana akampa mamaye. |
| 29 |
| Wanafunzi wake waliposikia habari, walikwenda, wakauchukua mwili wake, wakauzika kaburini. |
| 30 |
| Na mitume wakakusanyika mbele ya Yesu; wakampa habari za mambo yote waliyoyafanya, na mambo yote waliyoyafundisha. |
| 31 |
| Akawaambia, Njoni ninyi peke yenu kwa faragha, mahali pasipokuwa na watu, mkapumzike kidogo. Kwa sababu walikuwako watu wengi, wakija, wakienda, hata haikuwapo nafasi ya kula. |
| 32 |
| Wakaenda zao faragha mashuani, mahali pasipokuwa na watu. |
| 33 |
| Watu wakawaona wakienda zao, na wengi wakatambua, wakaenda huko mbio kwa miguu, toka miji yote, wakatangulia kufika. |
| 34 |
| Naye aliposhuka mashuani, akaona mkutano mkuu, akawahurumia; kwa sababu walikuwa kama kondoo wasio na mchungaji; akaanza kuwafundisha mambo mengi. |
| 35 |
| Hata zilipopita saa nyingi za mchana, wanafunzi wake walimwendea, wakasema, Mahali hapa ni nyika tupu, na sasa kunakuchwa; |
| 36 |
| uwaage watu hawa, ili waende zao mashambani na vijijini kandokando, wakajinunulie chakula. |
| 37 |
| Akajibu, akawaambia, Wapeni ninyi chakula. Wakamwambia, Je! Twende tukanunue mikate ya dinari mia mbili ili tuwape kula? |
| 38 |
| Akawaambia, Mnayo mikate mingapi? Nendeni mkatazame. Walipokwisha kujua wakasema, Mitano, na samaki wawili. |
| 39 |
| Akawaagiza wawaketishe wote, vikao vikao, penye majani mabichi. |
| 40 |
| Wakaketi safu safu, hapa mia hapa hamsini. |
| 41 |
| Akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama mbinguni, akashukuru, akaimega ile mikate, akawapa wanafunzi wake wawaandikie; na wale samaki wawili akawagawia wote. |
| 42 |
| Wakala wote wakashiba. |
| 43 |
| Wakaokota vipande vilivyomegwa vya kuweza kujaza vikapu kumi na viwili; na vipande vya samaki pia. |
| 44 |
| Na walioila ile mikate wapata elfu tano wanaume. |
| 45 |
| Mara akawalazimisha wanafunzi wake wapande mashuani, watangulie kwenda ng'ambo hata Bethsaida, wakati yeye alipokuwa akiwaaga mkutano. |
| 46 |
| Hata alipokwisha kuagana nao akaenda zake mlimani kuomba. |
| 47 |
| Na kulipokuwa jioni mashua ilikuwa katikati ya bahari, na yeye yu peke yake katika nchi kavu. |
| 48 |
| Akawaona wakitaabika kwa kuvuta makasia, kwa maana upepo ulikuwa wa mbisho; hata ilipopata kama zamu ya nne ya usiku akawaendea, akitembea juu ya bahari; akataka kuwapita. |
| 49 |
| Nao walipomwona anatembea juu ya bahari, walidhani ya kuwa ni kivuli, wakapiga yowe, |
| 50 |
| kwa kuwa wote walimwona, wakafadhaika. Mara akasema nao, akawaambia, Changamkeni; ni mimi, msiogope. |
| 51 |
| Akapanda mle chomboni walimo; upepo ukakoma; wakashangaa sana mioyoni mwao; |
| 52 |
| kwa maana hawakufahamu habari za ile mikate, lakini mioyo yao ilikuwa mizito. |
| 53 |
| Hata walipokwisha kuvuka, walifika nchi ya Genesareti, wakatia nanga. |
| 54 |
| Nao wakiisha kutoka mashuani, mara watu walimtambua, |
| 55 |
| wakaenda mbio, wakizunguka nchi ile yote, wakaanza kuwachukua vitandani walio hawawezi, kwenda kila mahali waliposikia kwamba yupo. |
| 56 |
| Na kila alikokwenda, akiingia vijijini, au mijini, au mashambani, wakawaweka wagonjwa sokoni, wakamsihi waguse ngaa pindo la vazi lake; nao wote waliomgusa wakapona. |
|
| Hifadhi Vidokezo |
https://beblia.bible:81/BibleAudio/swahili/mark/006.mp3
16
6