Wakati ule mliishi kufuatana na mtindo mbaya wa ulimwengu huu, mkawa mnamtii mtawala wa pepo wenye nguvu wa anga, pepo ambao huwatawala sasa watu wasiomtii Mungu.
Na hata sisi sote tulikuwa kama wao; tuliishi kufuatana na tamaa zetu za kidunia na kufanya tu mambo yale yaliyoipendeza miili na akili zetu. Kidunia, sisi kama vile pia wao, tulistahili ghadhabu ya Mungu.
Nyinyi mlio kwa asili watu wa mataifa mengine — mnaoitwa, “Wasiotahiriwa” na Wayahudi ambao hujiita, “Waliotahiriwa,” (kwa sababu ya kile wanachoifanyia miili yao) — kumbukeni mlivyokuwa zamani.
Wakati ule nyinyi mlikuwa bila Kristo; mlikuwa nje ya jamii ya Israeli; mlikuwa wageni na hamkuwa na sehemu katika yale maagano aliyoahidi Mungu. Mlikuwa bila matumaini na kama watu wasiomjua Mungu hapa duniani.
Maana Kristo mwenyewe ametuletea amani kwa kuwafanya Wayahudi na watu wa mataifa mengine kuwa jamii moja. Kwa mwili wake yeye mwenyewe aliubomoa ule ukuta uliowatenganisha na kuwafanya maadui.
Aliiondoa ile sheria pamoja na amri zake na kanuni zake, ili kutokana na jamii hizo mbili aumbe jamii moja mpya katika umoja naye na hivyo kuleta amani.
Basi, Kristo alikuja akahubiri Habari Njema ya amani kwenu nyinyi watu wa mataifa mengine mliokuwa mbali na Mungu, na pia kwa Wayahudi ambao walikuwa karibu na Mungu.