Kaka na dada, tuna jambo la kuwaambia juu ya kuja kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Tunataka kuzungumza nanyi juu ya wakati huo tutakapokusanyika pamoja naye.
Msikubali kufadhaishwa na kutiwa kuhofu ikiwa mtasikia kwamba siku ya Bwana tayari imekwishawadia. Wengine wanaweza kusema kwamba wazo hili limetoka kwetu katika jambo alilotuambia Roho, au tulilosema, au katika barua tuliyoiandika.
Msidanganywe na chochote wanachoweza kusema kuhusu kuja kwa Bwana. Siku hiyo ya Bwana haitakuja mpaka itanguliwe na kukengeuka kwa wanadamu na kumwacha Mungu. Na siku hiyo haitakuja mpaka ajitokeze kwanza Mtu wa Uovu, yule ambaye ana uhakika kuwa ataangamizwa.
Huyo atasimama kinyume na kujiweka mwenyewe juu ya kila kitu ambacho watu wanaabudu au kudhani kuwa kinafaa kuabudiwa. Ataenda na kuingia ndani ya Hekalu na kukikalia kiti cha enzi, akidai kuwa yeye ni Mungu.
Kisha huyo Mtu wa Uovu atatokea. Lakini Bwana Yesu atamuua kwa pumzi inayotoka katika kinywa chake. Bwana atakuja katika namna ambayo kila mtu atamwona, na huo utakuwa mwisho wa Mtu wa Uovu.
Mtu wa Uovu atatumia kila aina ya uovu kuwatia ujinga wote walio njiani kuelekea kuangamia. Wamepotea kwa sababu walikataa kuupenda ujumbe wenye ukweli kuhusu Yesu na kuokolewa.
Ndugu zangu, ninyi ni watu mnaopendwa na Bwana. Na imetupasa tumshukuru Mungu daima kwa sababu yenu. Hayo ndiyo tunayotakiwa kuyatenda, kwa sababu Mungu aliwaita kuwa miongoni mwa watu wa kwanza kuokolewa. Mmeokolewa na Roho aliyewafanya muwe watu wa Mungu walio watakatifu kupitia kuiamini kweli.
Tunaomba kwamba Bwana Yesu Kristo na Mungu Baba yetu awafariji na kuwaimairisha katika kila jambo jema mnalotenda na kusema. Mungu alitupenda na kutupa kupitia neema matumaini ya ajabu na faraja isiyo na mwisho.